Ahadi za Jakaya Kikwete Zaitesa CCM Kuelekea Uchaguzi 2015



Ahadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa wananchi katika mikutano mbalimbali nchini  wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, huenda zikawa mwiba kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu, kutokana na nyingi kutokutekelezwa au kuwa katika hatua za mwanzo.

Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, kwa nyakati tofauti alitoa ahadi kusaidia kuwakwamua wananchi kutoka kwenye dimbwi la umaskini, maradhi na kuboresha upatikanaji wa elimu nchini. Ahadi hizo zilitarajiwa kukamilika kabla hajatoka madarakani.

Ikiwa imebaki takriban miezi 10 ya uongozi wa kipindi cha pili cha awamu ya nne kufikia ukomo, muda unakwenda haraka na utekelezaji wa ahadi hizo unasuasua jambo linalotia shaka iwapo kila ahadi itatekelezwa kwa wakati.

Kushindwa kutekeleza ahadi hizo ambazo zimo katika kitabu cha ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za urais 2010, kilichondaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kunaiweka Serikali ya CCM katika wakati mgumu hasa pale itakaporudi kwa wananchi kutoa ahadi nyingine kwenye kampeni za uchaguzi mkuu ujao.