Zitto Kabwe awanyima usingizi CHADEMA, viongozi wahaha nchi nzima kuzima moto wa ACT


Wadau, hakika sasa si siri tena kwamba kitendo cha uongozi wa CHADEMA kumfukuza uanachama aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe kumekigharimu chama.

Mtakumbuka kuwa baada tu ya Tundu Lissu kutangaza kuwa Zitto Kabwe si mwanachama tena wa chadema baada ya Mahakama kufuta kesi aliyoifungua dhidi ya uongozi wake, Zitto Kabwe alitangaza kuachia madaraka ya ubunge na hatimaye kujiunga na ACT ambapo amechaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa chama hicho.

Kitendo hicho cha Zitto kuhamia ACT kilipokelewa kwa dhihaka na makada wa CHADEMA wakidhani kuwa Zitto Kabwe ndo anajimaliza kisiasa. Hata hivyo, baada ya Zitto Kabwe kuhamia ACT na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa chama hicho, alifanya ziara katika mikoa 10 nchini akiwa na viongozi wengine akiwemo Katibu Mkuu Samson Mwigamba. Umati uliofurika kuhudhuria mikutano ya ZITTO umewashtua sana viongozi wa CHADEMA. Kilichowashtua zaidi ni maelfu ya wafuasi wa chadema walioacha chama hicho na kujiunga na ACT.

Hakika Zitto Kabwe amechafua hali ya hewa ya Kinondoni Mtaa wa Ufipa. Sasa viongozi wanaona viti vinawaka moto. Sasa wanaona kuwa chadema inaelekea kwa Buriani. Ni kutokana na amsha amsha ya Zitto Kabwe na mchaka mchaka aliouanza, Viongozi wa CHADEMA hawana namna nyingine zaidi ya kukabiliana naye kwenye majukwaa na njia za siri.

Kwa upande wa majukwaani, Kamati Kuu ya chama hicho imeagiza kuwa viongozi wote wasambae mikoani kuzima moto wa Zitto Kabwe. Haijapata kutokea viongozi wakuu wote wakaikimbia ofisi ya CHADEMA kama ilivyo sasa. Kuanzia Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu wakuu wote wanapita maeneo aliyolisha sumu Zitto Kabwe ili kujaribu kutoa maziwa ambayo wanaamini pengine yanaweza kukata sumu hiyo. Lakini wapi.

CHADEMA sasa wanalia na kusaga meno. CHADEMA wanajutia maamuzi waliyofanya. Wataalam wa masuala ya siasa wanaona kuwa nguvu ya Zitto Kabwe katika kushawishi inazidi mara dufu uwezo wa viongozi wote wa UKAWA. Washauri wa CHADEMA akiwemo Saed Kubenea wanaona kuwa Zitto Kabwe akiachwa aendelee atasababisha nguvu ya UKAWA kumezwa na ACT.

Kwamba ACT itageuka kuwa chama kikuu ya Upinzani baada ya uchaguzi wa Oktoba 2015 ambao bila shaka CCM itashinda kwa kishindo. Aidha, jaribio la kumshawishi Zitto Kabwe kujiunga na UKAWA zinaelekea kugonga mwamba hasa baada ya John Mnyika kujichanganya alipotangaza kuwa Zitto Kabwe ni adui namba moja wa CHADEMA.

Imeandikwa na  Lizaboni/JF