Lowassa Azidi Kushawishiwa na Watu Mbali Mbali Atangaze Nia Ya Kuwania Urais

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Shija Ntelezu, ameungana na baadhi ya wana CCM wengine kumuomba Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, ajitokeze kutangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Ntelezu alisema kwa niaba ya wana Kishapu wenzake anamuomba Lowassa baada ya kumaliza adhabu aliyokuwa akitumikia yeye na wenzake watano ni wakati mwafaka hivi sasa wa kutangaza rasmi nia yake kugombea nafasi hiyo ili ampokee kijiti Rais Jakaya Kikwete.

Mwenyekiti huyo alisema kwa kadri anavyomfahamu Lowassa ni mmoja wa viongozi wachapa kazi wazuri hapa nchini na mwenye uwezo wa kutoa maamuzi magumu yanapohitajika kutolewa na kwamba ndiye kwa sasa anayeweza kumrithi Rais Kikwete na kuendeleza kasi ya kusukuma kasi ya maendeleo aliyoyaanzisha.

Alisema wakati taifa likielekea kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu ni muhimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikawa makini kuhakikisha kinamteuwa mgombea mwenye uwezo wa kukabiliana na wagombea wengine kutoka vyama vya upinzani.

“Sisi Kishapu tunaamini iwapo CCM itamsimamisha mgombea jasiri mwenye uzoefu wa kiuongozi ambaye pia ana historia nzuri ya uchapaji kazi hapa nchini ambaye haitokuwa kazi kubwa kumnadi kwa wapiga kura nafikiri Lowassa anatosha kwa nafasi hiyo hivi sasa, yapo mambo mengi makubwa aliyafanya wakati wa uongozi wake,”

“Utumishi wa Lowassa unafahamika hapa nchini kuanzia ndani ya chama hadi Serikalini, kwa sisi wa Shinyanga tunamfahamu zaidi maana aliwahi kuwa mtendaji wetu enzi ya TANU, lakini kikubwa tunachokikumbuka ni jinsi alivyowezesha kutufanikishia mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria,” alieleza Ntelezu.

Alisema ni muhimu vikao mbalimbali vya uteuzi ndani ya CCM vikawa makini katika kufikia maamuzi yake na wajumbe wake wasikubali kuyumbishwa na maneno ya watu wasiokitakia mema chama hicho na kwamba kimchunguze kwa umakini kila mgombea aliyejitokeza bila ya kumpaka sifa mbaya za uongo.

Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa ushauri wao wa kumtaka Lowassa agombee nafasi hiyo ya urais si kwamba wana CCM wengine waliojitokeza hawana sifa hizo, bali ni muhimu kumpa kipaumbele mtu mwenye uzoefu mkubwa wa kiutendaji ndani ya serikali na chama.

“Ushauri wetu usichukuliwe kwamba wana CCM wengine waliokwisha tangaza nia hawafai au hawana uwezo na hakuna anayewalaumu, maana ni haki yao ya kikatiba, lakini tunaangalia ni yupi miongoni mwao mwenye uwezo zaidi atakayeweza kukivusha chama chetu kwa urahisi kwenye uchaguzi mkuu ujao,” alieleza.

Akifafanua kuhusu uwezo wa Lowassa Ntelezu alitaja baadhi ya mambo makubwa aliyoyafanya alipokuwa waziri katika wizara mbalimbali nchini na pale alipokuwa waziri mkuu na kutaja baadhi ya shughuli kubwa kuwa ni pamoja na maamuzi ya ujenzi wa sekondari za kata ikiwemo ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Lowassa pamoja na makada wengine watano, Frederick Sumaye, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe na Stephen Wassira juzi walimaliza rasmi kifungo cha miezi 12 walichopewa na kamati kuu ya CCM ikiwa ni adhabu ya kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho na kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.