Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amefunguka na kusema
kuwa alipofukuzwa wanachama katika chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) alitamani kujiunga na Chama Cha NCCR-Mageuzi kwani ndicho
chama ambacho kilikuwa kinaendana na itikadi yake anayoifuata na
kuiamini ambayo ni itikadi ya Ujamaa. Zitto Kabwe amefunguka haya leo
alipokuwa akichat Live kupitia ukurasa wa facebook wa EATV katika
kipengele cha KIKAANGONI ambacho kimeanza upya katika msimu wa pili na
kitakuwa kikifanyika kila Jumatano kuanzia saa nane mchana mpaka kumi
Alasiri.
Zitto Kabwe alisema kuwa alishindwa kujiunga na Chama hicho cha
NCCR-Mageuzi kutokana na kuwepo kwa matatizo hivyo aliona siyo vyema
kujiunga nacho, ndiyo maana alifikiri kuwa na chama cha siasa ambacho
kitakuwa na misingi na itikadi ambayo yeye anaiamini na kuisimamia.