Mwigulu Nchemba apewa ‘Upako’ wa Urais


Askofu Mkuu wa Kanisa la General Mission Center Limited (GMCL) la jijini hapa, Nabii David Mpanji juzi alimkabidhi mafuta ya upako, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba kwa ajili ya kung’arisha nyota yake katika harakati zake za kuwania urais.

Nabii Mpanji alisema mafuta hayo yanaashiria ufalme na utawala na kusisitiza kwamba kitendo hicho ni kudhihirisha kuwa Nchemba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, anafaa kuliongoza Taifa.

Tukio hilo lilifanyika kwenye ibada maalumu iliyoambatana na harambee ya kuchangia vifaa vya redio ya kanisa hilo iliyoendeshwa na Nchemba na Sh53 milioni zilipatikana.

Alimtaka Nchemba kutamka nia yake ya kugombea urais mbele za watu, huku akisisitiza kuwa Taifa linahitaji mtu anayeweza kusimamia wananchi wenye kipato cha chini na kumtaja mbunge huyo wa Iramba Magharibi kuwa amethubutu kufanya hivyo.

“Mimi nasema wazee wasikuumize kichwa, hata Biblia inasema fahari ya wazee ni mvi zao lakini fahari ya vijana ni nguvu zao. Tunahitaji Watanzania wazalendo na jasiri ambao wanaweza kusema bila kuogopa kama wewe (Nchemba),” alisema.

Akizungumza katika ibada hiyo, Nchemba aliwashukuru Watanzania wenye imani naye na kubainisha kuwa muda ukifika atasema nia yake.

“Imebaki kitambo kidogo nitasema kwani mimi ni kiongozi wa chama, hivyo natakiwa kufuata taratibu na kanuni cha chama, nawaomba mvute subira kidogo nitasema tu,” alisema.

Nchemba alisema upako huo ni dalili tosha za Watanzania kutambua mchango wake katika kuwatumikia na yeye hatawaangusha... “Tutavuka mto tukifika mtoni.”

Mwigulu ambaye aliongozana na waimbaji maarufu wa nyimbo za Injili akiwamo Boniface Mwaitege na Moses Makondeko, alisema katika suala hilo (la urais) anamtegemea sana Mungu.

Aliwataka wananchi kuwa na uchungu na nchi yao kwa kutanguliza uzalendo kwani ni vigumu kupata kiongozi mzalendo katika Watanzania wasio kuwa na uzalendo.

Akisoma risala mchungaji wa kanisa hilo, Aquina Mhanze alisema mahitaji ya kanisa hilo ni Sh200 milioni kwa ajili ya kukamilisha vifaa vya redio na ofisi na kwamba kwa sasa kuna Sh15 milioni.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh150 milioni ni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya redio na Sh50 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya redio.