KIKAO cha viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kimeshindwa kuendelea baada ya baadhi ya wajumbe kushindwa kuafikiana kuhusu hoja iliyowasilishwa na Chama cha NCCR-Mageuzi, ya kutaka kujitoa kwenye umoja huo, imefahamika.
Viongozi hao walikutana jijini Dar es Salaam jana katika
Ofisi Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambapo pamoja na mambo mengine
walikuwa wakijadili hatima ya kuachiana majimbo kuelekea Uchaguzi Mkuu
wa Oktoba.
Katika kikao hicho ambacho kilitarajiwa kuanza saa 4
asubuhi kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake kilianza saa 6 mchana,
ajenda kuu zilikuwa ni kujadili namna ya kuachiana majimbo ambayo bado
mwafaka haujapatikana pamoja na utaratibu wa kumpata mgombea urais
kupitia Ukawa.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho
kilichokuwa chini ya Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kilishindwa kutoa mwelekeo
wa majimbo 18 yenye mvutano huku kila chama kikitaka kugombea kivyake.
Hata hivyo hoja hiyo iliibua mvutano mkali baina ya wajumbe
wa kikao hicho ambapo kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), ujumbe wake uliongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu
Mkuu Dk. Willibrod Slaa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu.
Kwa upande wa CUF, ujumbe wake uliongozwa na Profesa
Lipumba, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya na Naibu Mkurugenzi wa
Mipango na Uchaguzi, Shaweji Mketo.
NCCR-Mageuzi kiliongozwa na Mwenyekiti wake James Mbatia
ambaye baada ya kuwasilishwa hoja ya chama chake alishindwa kuendelea na
kikao na kulazimika kutoka nje ya ukumbi wa mikutano.
“Mwanzo tulianza kujadili suala la uandikishaji
wapigakura kwa mfumo wa BVR na changamoto zake zilizojitokeza pamoja na
hatima ya uwezekanao wa kuwapo kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.
“Pia tulijadili kwa kina mwendelezo wa ugawaji wa
majimbo yaliyobaki, lakini hata hivyo tuliacha ajenda hiyo kutokana na
kuibuka kwa hoja nzito kwa kila upande,” kilisema chanzo chetu ambacho hakikutaka kuandikwa jina lake.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinapasha kuwa
ilipotimu saa 7 mchana, aliingia Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Mbatia,
ambaye alishiriki katika hatua za awali za majadiliano hayo, lakini
ilipofika saa 9:20 aliondoka kabla kuwasilishwa hoja ya chama chake
kutaka kujitoa Ukawa.
Hata hivyo wajumbe walishindwa kuendelea na kikao hicho
kutokana na NCCR-Mageuzi kutokuwa na mjumbe ambaye angeweza kueleza kwa
undani sababu za kutaka kuchukua uamuzi wa kujitoa.
“Hoja iliyokuwa katika ajenda ni ya NCCR-Mageuzi
waliyowasilisha ya kutaka kujitoa Ukawa na dai lao kuu ni kutotendewa
haki kwa baadhi ya mambo, hasa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliopita.
“Na hili jambo si geni kwani mnapokuwa kwenye jumuiya
yoyote inawezekana ikatokea hali ya kutoelewana kwa baadhi ya wajumbe
kwa kuona kuna sehemu kuna mmoja anaona hajatendewa haki.
“Na jambo ambalo lilitakiwa ni kuzungumza na kulimaliza
ili watu wasonge mbele, na NCCR-Mageuzi walileta kama malalamiko… siwezi
kulizungumzia vizuri kwa sababu halijazungumziwa kwa undani kwenye
kikao,” kilisema chanzo chetu.
Mtoa habari wetu alisema kikao hicho kilitarajiwa
kumalizika jana usiku, lakini kutokana na hoja ya NCCR-Mageuzi,
ilimlazimu Mwenyekiti wa kikao hicho Profesa Lipumba kukiahirisha saa 11
jioni hadi leo ambapo kitaendelea.
Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi.
Hivi sasa joto la kuwatangaza wagombea urais ndani ya vyama
vinavyounda Ukawa pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) linazidi kupanda
huku kila upande ukimvizia mwenzake katika kutangaza mgombea nafasi
hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Ukawa katika
mkutano wao na wanahabari kueleza kuwa mgombea wao atatangazwa Machi
mwaka huu, lakini hadi sasa imepita miezi miwili bila kumtangaza.
Wakati hayo yakiendelea ndani ya Ukawa, CCM nayo hadi sasa
imeshindwa kueleza ni lini atapatikana mgombea wake pamoja na kutangazwa
kwa hatima ya makada sita wa chama hicho ambao wanadaiwa kuanza kampeni
kabla ya wakati.
Credit: Mtanzania