Mchezaji wa Yanga Hamisi Tambwe Ashinda Kesi na Kuvuna Mamilion ya Hela Simba


Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeitaka Simba kumlipa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe

kiasi cha Dola 7,000 (Sh 13,545,000) anazoidai klabu hiyo.

Simba jana ilipandishwa kizimbani kwa kesi tatu za madai ya fidia kwa waliokuwa waajiriwa wake ambao ni wachezaji Amissi Tambwe na Haruna Chonongo pamoja na kocha Zdravko Logarusic.

Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji chini ya mwenyekiti wake Richard Sinamtwa ilisikiliza shauri la Tambwe ambaye alikuwa anaidai Simba jumla ya kiasi cha Dola 7,000 zilizotokana na klabu hiyo kuvunja mkataba wake.

Simba ilitakiwa kumlipa Mrundi huyo fidia ya Dola 6,000 (Sh 11,610,000), pamoja na dola 1,000 (Sh 1,935,000) zikiwa ni malimbikizo ya mshahara wake.

Katika shauri hilo Simba iliyowakilishwa na Katibu wake Steven Ally, ilikubali kudaiwa na Tambwe, ambapo kamati ikiagiza malipo hayo yafanyike kwa awamu mbili ikitakiwa Aprili 30 kulipa Dola 5000 (Sh 9,675,000) kabla ya Alhamisi hii na kumalizia Dola 2,000 (3,870,000) ifikapo Mei 10, 2015.

Aidha kamati hiyo imeitaka Simba kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa makubaliano hayo kama watashindwa kufanya malipo hayo mapato ya mechi zake za mwisho yatashilikiliwa kulipa madeni hayo.

Mbali ya Tambwe, mwingine anayetarajia kuvuna fedha kutoka Simba ni winga wao Chanongo anayecheza kwa mkopo Stand United anayedai kutolipwa nusu mshahara wake kama ilivyokuwa katika makubaliano ya mkataba wake.