Wimbo wa Marehemu Kapteni Komba Wamliza Rais Kikwete

Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi na kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa machozi ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.

Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la “Nani Yule” ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu machozi iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo ni King Kiki, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.

Wakati wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo huo, idadi ya watu wanaolia ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu na jamaa wa marehemu.
Waombolezaji walisikika wakilia huku wakisema, “Jamani alikuwa akitunga nyimbo kuwaimbia wenzake waliofariki dunia, sasa leo anaimbiwa yeye.”