LICHA ya Serikali, jamii na jumuiya ya kimataifa kukemea ukatili dhidi
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), bado kuna wanaoendelea
kung’ang’ania mila potofu za kuamini kwamba bila ya ushirikina
unaohusishwa na matumizi ya viungo vya albino, hawawezi kufanikiwa
kimaisha, iwe katika kisiasa au kibiashara.
Hayo yanathibitishwa na kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya ukatili
dhidi ya albino, ambapo usiku wa kuamkia jana, watu wasiojulikana
walimshambulia na kumkata kiganja mtoto mwenye umri wa miaka sita,
Baraka Cosmas na kisha kutokomea nacho kusikojulikana.
Tukio hilo lililotokea katika kijiji cha Kipeta Bonde la Ziwa Rukwa
wilayani Sumbawanga, ambako mtoto huyo anaishi na wazazi wake, Cosmas
Yoram (32) na Prisca Shaaban.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa , Jacob Mwaruanda.
Alisema tukio hilo ni la saa 8 usiku wa kuamkia Jumapili wakati mtoto
huyo akiwa amelala na mama yake. Baba wa mtoto huyo hakuwepo wakati huo.
Akielezea zaidi, Kamanda Mwaruanda alisema usiku huo kikundi cha watu
wasiojulikana walivamia nyumba alimolala Baraka na mama yake mzazi,
Prisca wakiwa na silaha za jadi, ikiwemo mapanga na fimbo na kuanza
kumshambulia kwa kumcharaza viboko Prisca baada ya kukataa kuwapatia
mtoto huyo, mwenye ulemavu wa ngozi.
“Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo walimwamuru mama mzazi wa
mtoto Baraka kuwakabidhi mtoto huyo, lakini alikaidi ndipo walipoanza
kumshambulia kwa kumpiga kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na
kumjeruhi vibaya …
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana,” alibainisha.
“Waliingia ndani baada ya kuvunja mlango wa nyumba hiyo, ndipo katika patashika hiyo wavamizi hao walimkata mtoto Baraka kiganja cha mkono wake wa kulia na kuondoka nacho kusikojuliakana,” alibainisha.
Aliongeza kuwa wakati hayo yakitokea, baba mzazi wa mtoto huyo inadaiwa
alikuwa amelala katika nyumba ya mkewe mdogo kijijini humo.
Kwa mujibu wa Mwaruanda, mtoto huyo amelazwa katika katika Kituo cha
Afya cha Kamsamba wilayani Momba mkoani Mbeya kwa matibabu akiwa pamoja
na mama yake mzazi.
“Watu watatu ambao majina yao yamehifadhiwa, wanashikiliwa na Jeshi
la Polisi mkoani hapa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo
unaendelea ili kuwasaka wahusika na kiungo hicho cha kiganja cha mkono
wa mtoto Baraka,” alisisitiza Kamanda.