Tanzania Yetu na Viongozi Wenye Milioni Kumi za Mboga

VIONGOZI wamekuwa mstari wa mbele kuitangaza nchi hii kuwa ni maskini, na kwamba huyo ni adui wa kwanza kupambana naye akifuatiwa na ujinga na maradhi.

Kwa fikra ungedhani wanachokisema wanakimaanisha, kumbe hali haiko hivyo! Sitakosea nikisema umaskini wanaouzungumzia pengine ni wa wananchi siyo wa Tanzania kwa sababu nchi hii haijapata kuwa maskini wakati wowote.

Viongozi kwa mantiki, siyo wananchi. Hutaeleweka ukimuita waziri mwananchi; yeye mwenyewe atakushangaa na jamii itakushangaa pia kwa kuwa wananchi ni wakazi wa huko ushwekeni wanaolalia mihogo na majani ya maboga. Siogopi nikisema hivi!

Enzi za Mwalimu ilikuwa sawa, viongozi na watumishi wa umma kuitwa wananchi kwa sababu hawakuwa na tofauti ya mapato kama ilivyo hivi sasa. Mwenyekiti wa kijiji enzi hizo alishinda shamba akilima na kuvuna, leo kazi ya mwenyekiti ni kuwatisha Mamantilie na kujipatia fedha haramu.

Mawaziri wa utawala wa rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere waliagizwa kutoka ofisini na kutembelea vijiji vya ujamaa kushiriki kazi za kujenga taifa. Mawaziri wa siku hizi wengi wao wanashinda maofisini kucheza dili za kuihujumu nchi! Aibu.

Ni Tanzania hii ya Nyerere aliyekufa maskini ina wanaoweza kusimama hadharani na kutamka kuwa shilingi milioni 10 ni fedha za mboga! Je, viongozi kama hao watakuwa na kiasi gani ambacho watakiita cha ujenzi?

Milioni 10 alizoziita waziri wa zamani wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka kuwa ni mboga, eti ni sawa na za kununulia kisamvu sokoni, wakulima wa pamba watano watazihangaikia kwa mwaka mzima wakizitafuta kwa kupigwa na mvua na jua. Lakini waziri wa awamu hii anaziita fedha za mboga!

Kauli hii inaweza kuwa ya mshtuko kwa sababu imesikiwa na akina ‘yahe’ lakini ni ukweli ulio wazi kwamba, viongozi wengi serikalini kiasi hicho ni cha mboga, wenyewe wanajijua na serikali inaelewa kuwa ina sampuri ya viongozi wa namna hiyo.

Nina ushahidi wa hiki ninachokisema! Miaka kumi iliyopita nilikuwa na rafiki zangu ‘tulioshea’ mihogo ya kuchoma barabarani na kunywa ‘maji ya viroba’ lakini leo wanakula kwenye hoteli za nyota tano, kisa wamepewa nafasi za uongozi! Wanatumia fursa kujitajirisha.

Wakati hayo yanafanyika ukiingia kwenye katiba ya sasa utakutana na Ibara ya 132 ambayo inatambua uwepo kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma; kifungu kidogo cha kwanza kinatamka wazi pamoja na mambo mengine, sekretarieti hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza mienendo ya viongozi wa umma na kujiridhisha kama wanafuata maadili ya utumishi. Swali inafanya hivyo?

Tujiulize; ni lini hii sekretarieti hiyo ilishatoa ripoti kuwa tumemchunguza kiongozi fulani na kubaini amekiuka maadili na hivyo kupendekeza adhabu zichukuliwe dhidi yake?

Kama hakuna, ukimya wake unamaanisha viongozi hawajitajirishi kwa kutumia vyeo vyao? Na kama hivyo ndivyo hawa akina Tibaijuka na wenzake waliohojiwa juzi walikuwa wanafanya kazi mbinguni?
Nimesema mara nyingi, wizi wa mali ya umma siyo dhambi tena kwenye nchi hii, ikitokea umetajwa kuiba ujue hujaiba bali umekosana na wakubwa, hivyo wanakutoa kafara.

Kwa msingi huo hatuwezi kuongoza taifa kwa weredi kwa kufuata wakubwa wanataka nini, bali katiba yetu inatutaka tufuate miongozo ipi!  Tuwe fea, viongozi wameeneza mahekalu nchi nzima kila mtu anafahamu; wanahonga majumba mpaka kwa hawara zao, tumepata kuwauliza mali wametoa wapi? Au ndo ka-mfumo ka’ kula na kipofu kosa ni kumshika mkono? Nachochea tu!
GPL