Waziri Mpya wa Nishati na Madini, Simbachawene Ashikilia Msimamo wa Prof. Muhongo, Wazawa Hawawezi Kuwekeza kwenye Gesi

WAZIRI mpya wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amesema ni vigumu kupata mwekezaji mzawa katika kazi za uchimbaji wa gesi, kwa kuwa kazi hiyo ni gharama kubwa duniani na kampuni za uchimbaji gesi hazizidi kumi.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais Jakaya Kikwete Ikulu Dar es Salaam jana, Simbachawene alisema kauli kwamba wazawa hawawezi kuwekeza katika gesi, iliyotolewa na aliyemtangulia, Profesa Sospeter Muhongo, haikueleweka vizuri.

Alifafanua kuwa Watanzania wanaweza kuwekeza katika nyanja ya utoaji huduma kwa wachimbaji wa gesi na kuongeza kuwa mpaka sasa kuna maeneo ya huduma ambayo Watanzania wangeweza kuwekeza, lakini hawajafanya hivyo.

“Kuhusu kutoa vitalu kwa Watanzania kila mtu angependa kupewa kitalu cha gesi. Ukipata kitalu ndio umeshatoka, hata mimi ningependa kupata kimoja halafu nikitoka nakwenda Huston (Marekani) na kukiuza na kutoka,” alisema.

Alisema la msingi ni kuhakikisha mikataba ya uchimbaji gesi, inanufaisha Watanzania wote na katika kutoa huduma kwa wachimbaji, atapigania Watanzania wapate fursa ya kuwekeza huko. Alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi na kuongeza kuwa lakini katika ushirikiano huo, lazima kuwepo na uwiano kati ya ushirikiano na maendeleo ya wananchi.

Kuhusu jukumu la kusambaa umeme, Simbachawene alisema atachukua Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuanza nayo, ili kuhakikisha mafanikio ya usambazaji umeme yaliyopatikana chini ya uongozi wa Profesa Muhongo, yanaendelezwa na hatimaye Watanzania wote wapate umeme.

Naye Waziri mpya wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema anajua Watanzania wengi wanateseka kwa kunyang’anywa ardhi katika maeneo mbalimbali na hasa Dar es Salaam.

Amesema kwa kuwa amewahi kufanya kazi katika jiji la Dar es Salaam, ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa, anajua hali ya unyanyasaji katika ardhi ilivyo na kuwataka Watanzania wenye matatizo na ardhi, kutoa taarifa ili wasaidiwe.

Lukuvi alikiri kukabiliwa na changamoto ya baadhi ya watendaji wasio waaminifu katika sekta hiyo na kuongeza atajitahidi kukabiliana na changamoto hiyo kwa uaminifu.
Chanzo:Habarileo.