Baadhi ya wanaobeza, wanadai kwamba Makonda hana sifa ya kuongoza wilaya kubwa kama Kinondoni, ambayo ina changamoto na migogoro mingi ya ardhi.
Makonda ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM, jina lake limekuwa kubwa hivi karibuni baada ya kutuhumiwa kumpiga Jaji Warioba wakati wa mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Pia, kujitokeza kwake hadharani kumpinga Edward Lowassa, kuliongeza jina hilo kuwa maarufu.
Wakizungumza na Mpekuzi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wasomaji wa mtandao huu, wamedai kuwa uteuzi huo wa Rais ni mzuri ila alikosea kumweka wilaya ya Kinondoni yenye matatizo chungu mzima ya kiutendaji ikiwemo migogoro ya mipaka, ardhi, wafanyabiashara ndogondogo na mambo mengine ya ndani.
“Tunampongeza Rais kwa kuteua wakuu wapya wa wilaya, ila kwa huyu Paul Makonda kumweka Kinondoni, ameteleza. Hii wilaya inahitaji mtu mwenye uzoefu mkubwa katika uongozi na uadilifu” alisema Sued Musa.
Naye Albert Chenza wa Dar alikuwa na haya ya kusema: "Ma-DC kama Makonda wapo kwa ajili ya CCM kutetea maslahi ya CCM au wapo kwa ajili ya wananchi kuwasaidia wananchi?
"Ikumbukwe DC ndiye Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na DSO akiwa katibu wake, sasa mtu kama Makonda ambaye yupo tayari kufanya vurugu yoyote kutetea maslahi ya CCM leo kupewa u-DC wa Kinondoni tutegemee nini uchaguzi mkuu wa Oct 2015?
"Ikitegemea kuna mvutano kati ya wapinzani na CCM ambao vyombo vya usalama vinatakiwa kuleta haki na amani, wapinzani wategemee kupata haki au NGUVU zao ndo itakuwa haki yao? Hakika nuru ya amani inafifia Tanzania.
"Hii ni kama tupo disco la kukesha ambalo inatolewa CD hii inawekwa ile na zote unahitaji unywe panadol kuzisikiliza." Alisema Albert na kuongeza:
"Ni dhahiri sasa Mzee Warioba na Taasisi ya Mwalimu Nyerere wamemjua adui yao halisi ni nani. Aliyekua mstari wa mbele kumshambulia na kumfanyia fujo Mzee Warioba amepongezwa rasmi kwa kupewa ukuu wa wilaya.
"Pia imeendelea kujidhihirisha sasa kuwa Ukitaka U-DC wewe mtukane Lowassa kama Nape Nnauye, Mrisho Gambo na Makonda walivyofanya.
"Na pengine atakayekua jasiri vya kutosha na kumchapa angalao vibao viwili usoni anaweza kupata Ukuu wa Mkoa au Ubalozi kabisa"
Sailas Kassa Edward yeye anamaoni tofauti kidogo, na hapa anaanza kwa kumpongeza Makonda: "Siku ya jana (juzi) Rais kikwete alifanya uteuzi wa wakuu wa wilaya ambapo moja ya wateule ni paul Makonda.
"Inanishangaza sana kutoka jana(juzi) mpaka leo(jana) watanzania wamekuwa wakilalamika kupitia mitandao ya kijamii wakikosoa uteuzi wa ndgu makonda.
"Mimi binafsi nampongeza kwa nafasi aliyopata nadhani katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania haijampa rais mamlaka ya kuwatenga watu bali kila mtu ana haki ya kuongoza na pia kuongozwa.
"Kwa watanzania itafika hatua kila mtu mwenye intrest za chama cha mapinduzi hamtaki apate nafasi je nani ana haki na nani hana?
"Nimejaribu kuchunguza haya yote yanatoka wapi mpaka makonda anakuwa gumzo mtaani nikagundua kuwa wapenzi wa Edward Lowassa wameumia sana kuona makonda anakuwa mkuu wa wilaya hasa ukizingatia anafichua mbinu na hila za Lowassa na makundi yake. "