Shule Binafsi Zatesa Matokeo Kidato cha Nne, Shule za Vipaji Maalumu Zaendelea Kuporomoka

Dar es Salaam. Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe na za seminari zimeendelea kuporomoka.


Katika matokeo hayo, Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho.

Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.