Huyu ndio ‘Karani’ wa Benki Anayeuza Figo yake apate mtaji wa Kufanya Biashara

Si ajabu kusikia mtu amejiua kwa sababu tu ya ugumu wa maisha. Wengi wanafikia uamuzi huo baada ya kuhisi hawana msaada mwingine wa kupunguza makali ya maisha. Hata hivyo, kujiua siyo njia sahihi ya kupambana na changamoto.


Hali imekuwa tofauti kwa kijana Armstrong Bangili aliyeahirisha uamuzi wake wa kutaka kujinyonga na sasa anafikiria kuuza figo yake. Anasema anaishi maisha ya tabu tangu alipofukuzwa kazi katika benki moja mwaka 1998.

Kabla ya kutekeleza ‘jaribio la kujiua’ wiki iliyopita, Bangili alisoma Gazeti la Mwananchi, toleo la Januari 3. Alipokutana na habari ya Andrew Chimulimuli kutoka Morogoro aliyetangaza kuuza figo yake kwa Sh90 milioni.

Anasema alipata tumaini kuwa hata yeye anaweza kuuza figo yake na kuondokana na umaskini unaomkabili kwa sasa. Hata hivyo, anakiri kuwa hana elimu yoyote juu ya athari za kutoa figo au jinsi ya kuishi baada ya kutoa figo.

“Nimeamua kuuza figo ili nipate pesa za kufanya biashara. Figo yangu naiuza kwa Sh50 milioni tu, bei yangu ni poa kabisa, siyo kama huyu jamaa,” anasema Bangili huku akionyesha makala ya Chimulimuli ambayo ilimbadili mawazo.

Bangili mwenye umri wa miaka 45 anasema amekuwa akiishi kwa kuombaomba miaka yote, jambo linalowakera watu na yeye pia. Anaeleza kuwa amejaribu kutafuta kazi maeneo mbalimbali lakini amekosa.

Anabainisha kuwa akipata fedha hizo ataanzisha mradi wa kilimo cha mbogamboga na ufugaji wa nyuki. Anaamini kuwa ana uwezo wa kuendesha shughuli hiyo na kujiongezea kipato zaidi ndani ya muda mfupi.

“Yaani nikipata hiyo hela nitanunua shamba la ekari tano huko Bagamoyo au Tegeta, nitaanzisha kilimo cha mbogamboga na kufuga nyuki. Baada ya miaka mitatu mbona nitakuwa bilionea!” anasema huku akicheka.

Kijana huyo anayeishi Sinza, Dar es Salaam anaonekana kudhoofu mwili akisema hiyo inatokana na kula mlo mmoja na wakati mwingine kutokula kabisa. Anasema mbali na kuwa ndugu zake hawana uwezo, pia wamemchoka kwa sababu wamemsaidia kwa muda mrefu.

Bangili anatoka kwenye familia ya watoto wanne, akiwa ndiye mkubwa. Anasema wadogo zake wengine wana maisha yao na wanajimudu kwa kipato kidogo wanachokipata.

Mara nyingi amekuwa akipokea msaada kutoka kwa waumini wa Kanisa la Waadventisti wa Sabato, lakini anasema sasa amechoka kuombaomba, anahitaji kuwa na kazi ya kumuingizia kipato.

“Nataka nikipata pesa nioe, umri nao umekwenda. Nashindwa kuoa kwa sababu sina pesa za kumtunza mwanamke,” anasema Bangili ambaye ana elimu ya kidato cha nne.