IGP: Jina la Mchinjaji wa ISIS Jihadi John Halikuwepo Kwenye Database ya Polisi Tanzania Kama Inavyoripotiwa

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Kamanda Ernest Mangu, ameliambia gazeti la The Citizen kuwa jina la Mohammed Emwazi maarufu kama Jihadi John halikuwepo kwenye database ya watuhumiwa wa kigeni waliokamatwa na kuondolewa nchini mwaka 2009. Kanusho hilo limeripotowa pia na BBC News.

Hata hivyo, Kamanda Mangu alisema kuwa hawezi kusema kwa uhakika kama Jihadi John alishikiliwa na maafisa wa usalama nchini kwa sababu watuhumiwa wa aina yake ni mabingwa wa kudanganya na wanaficha identity zao na hufoji pasi za kusafiria. Gazeti hilo lilijaribu kumtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCP Diwani Athumani, lakini hawakupatikana.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwa Jihadi John alitaka kuingia Tanzania mwaka 2009 kwa kutumia jina la Muhammad ibn Muazzam. Alikuwa anasafiri na Mwingereza mwingine kwa jina Abu Talib na Mjerumani aliyeitwa Omar. Hata hivyo, alizuiliwa kuingia nchini mara tuu baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Taarifa zinadai kuwa maafisa wa usalama wa Tanzania walimkamata, wakamhoji, wakamweka ndani na kesho yake wakampakia kwenye ndege na kumrudisha kwao Uingereza kupitia Holland. Gazeti la The Independent la Uingereza linadai kuwa Jihadi John alikamatwa nchini kwa amri ya MI5 ya Uingereza.