Samatta ampa ushauri Msuva

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayechezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mbwana Samatta, amesifu kiwango cha Simon Msuva wa Yanga akisema kinafaa kuchezea klabu za Ulaya.



Akifafanua kauli yake hiyo, Samatta alisema Msuva ni mchezaji mwenye malengo ya kufika mbali na hilo linatokana na juhudi na mikakati yake aliyokuwa anaipanga wakati wanacheza pamoja timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, iliyokuwa inanolewa na Kim Poulsen.

“Tukiwa timu ya taifa ya vijana nilikuwa nakaa naye chumba kimoja, amewahi kuniambia atahakikisha anajituma na kunuia kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Ni mchezaji anayependa kujifunza kutoka kwa wengine, naamini juhudi zake hizo ndizo zilizomfikisha pale alipo kwa sasa,” alisema.

Aligusia pia kuhusiana na viongozi wa timu husika kwamba wanatakiwa kuwatafutia wachezaji nafasi za kucheza nje ya nchi jambo litakalosaidia kupata wachezaji wazuri katika timu ya taifa kwa sababu wanakuwa wamejifunza mambo mengi.

“Pamoja na Msuva kutakiwa kupanua mtandao mkubwa wa kufika mbali, pia kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ni vizuri zikajitahidi kuwauza wachezaji wao kwa faida ya maendeleo ya klabu hizo na taifa kwa ujumla, “ alisema.

Mpaka sasa Samatta amebakiza mwaka mmoja katika mkataba na klabu yake ambapo alieleza kuwa mipango yake ni kutimkia Ulaya. Alisema mawakala wake wapo kwenye mazungumzo na timu yake na wakifikia mwafaka ataondoka.

Amedokeza huenda akaenda Ujerumani, Urusi au Ufaransa.