NIMR Yatengeneza Dawa ya Asili ya Ukimwi..Kuingizwa Sokoni Hivi Karibuni

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imetengeneza dawa za asili zilizoboreshwa kwa ajili ya tiba kwa magonjwa mbalimbali, ikiwemo Ukimwi baada ya kuzifanyia utafiti kubaini uwezo na usalama wake.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk Mwele Malecela amesema iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa dawa asilia 11 ziingizwe sokoni.

Magonjwa mengine ambayo dawa hizo zilizoboreshwa zitatumika kwa ajili ya tiba ni kisukari na kupunguza mafuta (lehemu) mwilini, uvimbe wa tezi dume kwa wanaume na dawa inayoongeza nguvu za kijinsia kwa wanaume.

Dk Mwele alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka 35 ya utafiti na maendeleo ya afya na kusema tafiti katika tiba asilia zilifanyika kubaini uwezo na usalama wa dawa hizo zinazotumiwa na jamii mbalimbali hapa nchini.

“Aidha taasisi imefanya utafiti kwa kuzingatia uwezo na usalama kwa watumiaji na kufanikiwa kutengeneza dawa asili zilizoboreshwa kwa ajili ya tiba kwa magonjwa ya malaria, Ukimwi na magonjwa nyemelezi, ugonjwa wa ini, shinikizo la damu…,” alisema.

Alisisitiza, “taasisi iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa dawa asilia 11 ili ziweze kuingizwa sokoni.”

Akizungumzia tatizo la kupungua kwa nguvu za kiume, alisema linaonekana ni kubwa na hata katika maonesho wanayofanya, dawa inayoimarisha nguvu hizo hununuliwa zaidi.

Aidha alisema iko haja kwa wadau na serikali kuwekeza nguvu zaidi katika taasisi hiyo kufanya tafiti zitakazosaidia kugundua chanzo na tiba ya tatizo la uvimbe kwa matumbo ya uzazi ya wanawake wengi wenye asili ya kiafrika.

Kuhusu ugonjwa wa malaria, Dk Mwele alisema matokeo ya tafiti yanaonesha kupungua maeneo ya Kaskazini, Kaskazini-Mashariki, Kanda ya Kati na Kanda ya Ziwa Victoria kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya vyandarua na uelewa wa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira.

Alisema utafiti wa chanjo ya malaria uliofanywa katika wilaya za Bagamoyo na Korogwe umeonesha uwezo mkubwa wa kinga kwa watoto.

Alisema taasisi inaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kufuatilia na kutathmini usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vinavyotumika katika vyandarua na katika kunyunyizia ukoko kwenye nyumba.

Alisema taasisi imeendelea kuishauri Serikali katika kuainisha mbinu sahihi za kupambana na usugu huo ambapo pia matokeo ya tathmini za ubora wa dawa za tiba ya malaria yameonesha kuwa dawa mseto ya ALU bado inao uwezo mkubwa wa kutibu ugonjwa wa malaria.